“Katika yote, Kupenda na Kutumikia” (Mt. Inyasi wa Loyola, 1491 – 1546)
Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Maria–Theresa Ledochowska au Parokia ya Kiwanja cha Ndege ni mojawapo ya Parokia za Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Kufuatia Sensa ya mwaka 2012/2013, parokia kuu (K/Ndege) ina waamini hai wapatao 8,561. Parokia Ndogo ya Mtakatifu Inysi wa Loyola - Miyuji Kusini, ina waamini wapatao 1,712. Jumla kuu ni waamini 10,273. Parokia ya Kiwanja cha Ndege imezungukwa na Parokia za Makole, Nkuhungu, Mbwanga, Kanisa Kuu, Veyula na kizota ambazo kwa pamoja zinaunda Dekania ya Mt. Paulo wa Msalaba.
Parokia ilianzishwa mwaka 1976 kama Jumuia Ndogo Ndogo iliyokuwa ikiabudu kwa pamoja kwa kutumia madarasa ya shule ya msingi ya Kiwanja cha Ndege. Kanisa la kwanza lilijengwa kwenye viwanja vya Parokia mwaka 1977 na hapo ndipo utume wa vijana ulipoaanzia na baadae kanisa likabarikiwa rasmi siku ya tarehe 15 Oktoba 1978.
Ongezeko la idadi ya waamini lilipelekea ujenzi wa Kanisa linalotumika kwa sasa. Ujenzi ulianza mwaka 1979, na Kanisa lilibarikiwa mwaka 1984. Leo hii parokia inazo Jumuia Ndogo Ndogo 45.
Kwa nini Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska?
Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska ni mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Mt. Petro Klaveri (Sisters of St. Peter Claver) waishio Roma, Italia. Masista hawa walitoa ufadhili mkubwa wa ujenzi wa Kanisa letu. Jina hili ni kwa heshima ya Mwanzilishi wa Shirika lao, Maria-Theresa Ledochowska. Sikukuu ya kumkumbuka Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska huadhimishwa kikanisa tarehe 6 Julai. Hii pia ni siku ya Parokia yetu.
“Mikono miwili iliyo tayari kutoa” (Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska, 1863 – 1922).
0 comments:
Post a Comment